15 Aprili 2025 - 22:07
Source: Parstoday
Trump au mkoloni muflisi? Ukosoaji mkali wa mchumi wa Ufaransa dhidi ya sera za Marekani

Gazeti la Ufaransa la "Le Monde" limekosoa sera za serikali ya Marekani katika kuamiliana na nchi nyingine na kuandika: "Mgogoro uliopo si wa kiuchumi tu, bali pia ni mgogoro wa uhalali na utendaji wa kisiasa, unaotokana na uozo wa muundo wa madaraka nchini Marekani."

Sera za Rais wa Marekani, Donald Trump katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuzidisha ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani na kuchukua hatua kali hata dhidi ya washirika wake, zimeibua hisia kali kutoka kwa nchi nyingi, na wengi wanaamini kwamba Marekani si nchi ya kutegemewa tena kwa washirika wake. Wakati wa vita dhidi ya Iraq, Marekani ilidhihirisha wazi kuwa iko tayari kuivamia nchi nyingine kinyume cha sheria ili kulinda maslahi yake, na sasa maslahi hayo yamedhihirika katika kutoza ushuru wa ziada wa forodha dhidi ya bidhaa za nchi nyingine.

Thomas Piketty, profesa katika Chuo cha Uchumi cha Paris, amezungumzia sera za Trump katika dokezo kwenye gazeti la Le Monde na anaamini kuwa Marekani, chini ya sera ya Trump na wafuasi wake, kwa sasa inakusudia kudumisha uchumi wake kwa kutoza ushuru ziada, ambao anautaja kama uhujumu wa Marekani, dhidi ya mataifa mengine duniani ili kufidia nakisi kubwa ya bajeti ya nchi hiyo. Anasisitiza kuwa, Matrumpist hawajui ukweli kwamba nguvu ya Marekani imeshuka na kwamba hata China mnamo 2016 ilikuwa na Pato Ghafi kubwa zaidi kuliko Marekani.

Trump au mkoloni muflisi? Ukosoaji mkali wa mchumi wa Ufaransa dhidi ya sera za Marekani

Thomas Piketty

Kwa mujibu wa Piketty, Marekani inasumbuliwa na upungufu mkubwa wa ushawishi wake kimataifa, kiuchumi na kisiasa. Anaamini kuwa mabadiliko haya hayatokani tu na matukio ya hivi karibuni, bali ni hitimisho la masuala ya muda mrefu, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa kijeshi wa Marekani katika nchi mbalimbali kama vile vita vya Iraq, ambavyo vilisababisha hasara za roho za maelfu ya watu na kukosekana utulivu wa kikanda.

Profesa katika Chuo cha Uchumi cha Paris amesisitiza kwamba mgogoro wa sasa unatoa changamoto kwa kituo cha nguvu za kiuchumi, kifedha na kisiasa cha Marekani. Kubwa zaidi kuliko hilo ni mrundikano wa nakisi ya biashara na deni la nje la Marekani la umma na la binafsi, ambalo hadi mwaka 2025 limefikia karibu 70% ya Pato la Taifa.

Kupanda kwa viwango vya riba kunaweza kuilazimisha Marekani kulipa mtiririko mkubwa wa faida kwa mataifa mengine duniani, jambo ambalo hadi sasa imelikwepa kutokana na udhibiti wake juu ya mfumo wa kifedha wa kimataifa.

Inatupasa kusema kuwa, Trump anataka kujaza hazina ya nchi yake kwa kunyakua madini ya Ukraine, Greenland na Mfrereji wa Panama, lakini Donald Trump kimsingi si chochote zaidi ya kiongozi wa kikoloni aliyefilisika, kwa sababu Marekani haina tena meno na uwezo wa kiuchumi iliokuwa nao dhidi ya nchi nyingine.

Trump au mkoloni muflisi? Ukosoaji mkali wa mchumi wa Ufaransa dhidi ya sera za Marekani

Viongozi wa kundi la BRICS

Mchumi huyo wa Ufaransa anaendelea na maelezo yake kwa kuashiria mataifa mengine yanayoinukia kiuchumi duniani, kama vile kundi la BRICS na nchi za Global South, ambazo Marekani haina ubavu wa kuzitwisha matakwa na siasa zake.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha